Tupo Kamili Kuivaa RS Berkane

Leo saa nne usiku kikosi chetu kitashuka katika Manispaa ya Berkane tayari kwa mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.

Ni mchezo ambao utatoa taswira nzima ya timu gani itakuwa na nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa michuano hii msimu huu.

Ni mchezo ambao tunautazama kwa jicho la tatu tukiwa na malengo yetu ni kupata matokeo chanya ili mechi ya marudiano nyumbani tuwe kwenye nafasi nzuri ya ushindi na tusicheze kwa presha.

Hii ndio kauli ya Fadlu…..

Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema tunaenda kukutana na timu yenye uzoefu wa mashindano haya na wapo kwenye kiwango bora kwa sasa lakini tumejipanga kuchukua tahadhari zote zinazotakiwa ili kuwadhibiti.

Fadlu ameongeza kuwa amewaandaa wachezaji kimwili na kiakili kuwa watakutana na mashambulizi ya haraka haraka kutoka kwa Berkane na wanatakiwa kuwa wastahimilivu na watulivu ili kuweza kupata kupata matokeo chanya.

“Tumejipanga kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa fainali, kikosi chetu ni kichanga kwenye michuano hii ukilinganisha na wapinzani wetu lakini tumejipanga vizuri na malengo yetu ni kushinda taji hili,” amesema Fadlu.

Wachezaji wanautaka ubingwa….

Nae mlinzi wa kati, Che Fondoh Malone amesema ubingwa wa michuano hii ni fahari ya kila mchezaji wa Simba na wapo tayari kupambana hadi mwisho kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kikosi kilichoweka historia ya kuchukua taji hilo.

“Kila mchezaji ana ndoto ya kucheza fainali ya michuano hii mikubwa Afrika, tunafahamu tunaenda kukutana na mpinzani mkubwa lakini tupo tayari kupambana hadi mwisho kufanikisha malengo ya timu,” amesema Che Malone.

Walitufunga kwao, tukawafunga kwa Mkapa

Mwaka 2022 tulikutana na Berkane kwenye michuano hii lakini ilikuwa katika hatua ya makundi.

Mchezo wa kwanza ulipigwa Februari 27, katika Uwanja wa Manispaa ya Berkane tulipoteza kwa mabao 2-0 na mechi ya marudiano iliyopigwa Benjamin Mkapa, Machi 13 tuliibuka na ushindi wa bao moja.

SHARE :
Facebook
Twitter

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

GET NEWSLETTER