Leo saa moja usiku kikosi chetu kitashuka katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuikabili Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Tunaingia kwenye mchezo wa leo tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao moja tuliopata dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi ya ugenini iliyopigwa katika dimba la Jamhuri, Mei 17.
Ushindi katika mchezo wa leo ni muhimu kwetu kwakuwa tunahitaji kumaliza nafasi ya pili ili kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha Mgunda azungumzia maandalizi ya mchezo…..
Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda amesema kikosi kimejipanga kucheza mechi ngumu kutoka kwa Geita lakini anaamini wachezaji watafuta maelekezo watakayowapatia.
“Maandalizi ya mchezo wa kesho dhidi ya Geita yamekamilika, tunafahamu utakuwa mchezo mgumu kutokana na Ligi kuelekea ukingoni lakini tupo tayari kupambana ili kupata ushindi,” amesema Mgunda.
Chama, Miqussone wako tayari kwa Geita
Nyota wetu wawili Clatous Chama na Luis Miqussone wameshiriki mazoezi kamili pamoja na wenzao na wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo.
Viungo hao washambuliaji wamekosa mechi kadhaa kutokana nakuwa majeruhi lakini sasa wako fiti na benchi ufundi likiona inafaa wanaweza kuwatumia leo.
Lakred afanya mazoezi kamili na timu….
Mlinda mlango Ayoub Lakred ambaye alikosekana katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kutokana na maumivu nae amerejea kikosini na amefanya mazoezi kamili na yupo tayari kwa mechi ya leo.
Tuliwafunga mara ya mwisho Kirumba…..
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Februari 12 tuliibuka na ushindi wa bao moja.
Bao hilo lilifungwa dakika ya 83 na kiungo mkabaji Babacar Sarr baada ya kupokea pasi kutoka kwa Kibu Denis.