Wakati michuano ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ikianza leo katika Uwanja wa Azam Complex wadhamini wakuu wa Kikosi chetu cha vijana MobiAd wamekuja na Kampeni ya ‘Twenzetu Chamazi’.
Lengo ya Kampeni hii ni kuhamasisha mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Azam Complex kuipa sapoti timu ili kufanya vizuri ikiwezekana tuchukue ubingwa.
Muwakilishi wa MobiAd, Baraka Mohamed amesema Kampeni ya Twenzetu Chamazi itawezesha mashabiki kujua kila kitu kinachoendelea uwanjani kupitia ‘MobiAd Soccer’ ambapo ratiba, wafungaji itakuwa inawekwa kupitia simu za mikononi.
“Tunaenda kuanza michuano ya vijana na kesho tutacheza na Kagera Sugar, tumezindua kampeni ya ‘Twenzetu Chamazi’ kwa ajili ya mashabiki kuja kuisapoti timu yetu, malengo yetu ni kuhakikisha tunachukua ubingwa.
“Kwa wale mashabiki ambao wapo nje ya Dar es Salaam watakuwa wanapata taarifa za moja kwa moja za ratiba, wafungaji kupitia MobiAd Soccer,” amesema Baraka.
Kwa upande wake shabiki kindaki ndaki wa timu yetu Agnes Daniel ‘Aggy Simba’ amesema kwa upande wao wapo tayari kuhamasisha wengine kujitokeza kwa wingi.
Kwa upande wake Mikoi Kisugu amewashukuru wadhamini MobiAd kwa kuwekeza kwa vijana ambao ndio chimbuko la soka ili kupata mafanikio.
“Sisi kama mashabiki tupo tayari kwenda Chamazi kuipa sapoti timu yetu, popote Simba inapokuwepo sisi tupo na Wanasimba wenzetu tunawaomba mje kwa wingi Chamazi kuishangilia timu ili tuibuke na ushindi,” amesema Kisugu.