Kocha Mkuu, Didier Gomez amesema katika mchezo wa kesho wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merrikh atacheza soka la kushambulia kwa sababu tupo nyumbani.

Gomez amesema anategemea kufanya mabadiliko kidogo ya kikosi hasa kwenye safu ya ushambuliaji ili kuhakikisha tunashambulia ili kupata alama zote.

Kocha Gomez amesisitiza kuwa pointi tatu za kesho ni muhimu kwa kuwa zitatuweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia robo fainali ambapo tutahitaji kupata alama moja kwenye mechi zetu mbili zilizobaki.

“Tutacheza soka la kushambulia sababu tupo nyumbani, tunahitaji kushinda mechi ya kesho ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuingia robo fainali,” amesema Kocha Gomez.

Kuelekea mchezo huo Kocha Gomez amesema tutamkosa mlinzi wa kati Pascal Wawa kutokana na kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano lakini wengine wote wako tayari.

“Mchezaji pekee tutakayemkosa ni Wawa sababu ya kutumikia adhabu ya kadi tatu za njano. Ila tunao Peter Muduhwa, Erasto Nyoni na Kennedy Juma ambao wanaweza kuziba nafasi yake,” amesema kocha Gomez.