Kocha Mkuu, Fadlu Davids amesema kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tabora United utakaopigwa Uwanja wa KMC kesho saa 10:15 jioni.
Kocha Fadlu amesema kikosi chetu tayari kimepata wiki sita za mazoezi pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki pamoja zile za Ngao ya Jamii.
Kocha Fadlu ameongeza kuwa malengo yetu ni kuhakikisha tunaanza vizuri ligi kwa kuanza na ushindi dhidi ya Tabora kesho.
“Timu ipo tayari kwa kuanza Ligi Kuu, kikosi chetu kipo kwenye umbo bora la kiushindani na mawasiliano ndani ya uwanjani yameendelea kuimarika.
“Leonel Ateba amejiunga nasi juzi amefanyiwa vipimo vya afya na amefanya mazoezi ya jioni kwahiyo inategemea na utimamu wake wa mwili kama ataweza kuwa sehemu ya mchezo wa kesho,” amesema Fadlu.
Kwa upande wake mlinda mlango, Hussein Abel amesema wao kama wachezaji wamejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Tabora.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari, tunaamini utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda,” amesema Abel.